Jumanne , 24th Jun , 2025

Iran inasema iko tayari kuacha mashambulio, iwapo Israel nayo itaacha kuishambulia, saa chache baada ya rais wa Marekani Donald Trump kutangaza kuwa nchi hizo mbili zilikuwa zimekubaliana kusitisha vita.

Waziri wa Mambo ya nje wa Iran Abbas Araghchi amesema tayari nchi yake imesitisha mashambulio kuanzia leo Jumanne Alfajiri na inataka Israel nayo ichukue uamuzi huo.

Hata hivyo, jeshi la Israeli limesema Iran imeendelea kuishambulia kwa kuendelea kurusha makombora yake, lakini halijasema muda wa  mashambulio hayo.

Rais Trump naye kupitia mitandao yake ya kijamii, alitangaza kuwa Israel na Iran zilikuwa zimekubaliana kusitisha vita kwa hatua ndani ya saa 24 zijazo, kuanzia saa 10 Alfajiri saa za Kimataifa, siku ya Jumanne.

Trump amesema Iran itakuwa ya kwanza kusitisha mashambulio yake yote na  kufuatwa na Israel baada ya saa 12, na kuongeza kuwa pande zote zimekubaliana kudumisha amani na kuheshimiana.

Tangazo hili la Trump limekuja baada ya Iran kurusha makombora kulenga kambi ya jeshi la angaa ya Marekani ya Al Udeid nchini Qatar, mashambulio ambayo yalidhibitiwa angani na kutosababisha madhara yoyote.