Jumapili , 28th Sep , 2025

Vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran vimerejeshwa rasmi usiku wa manane siku ya leo Jumapili, Septemba 28, kufuatia kushindwa kwa mazungumzo na nchi za Magharibi na mashambulizi ya Israel na Marekani katika maeneo yake ya nyuklia.

Rais wa Iran amekosoa madai ya Marekani ya kukabidhi uranium yote iliyorutubishwa wakati taifa hilo likilaani kurejeshwa kwa vikwazo vya Umoja wa Mataifa juu ya mpango wake wa nyuklia.

Rais Massoud Pezeshkian alisema jana Septemba 27 kwamba Marekani iliitaka Iran ikabidhi uranium yake yote iliyorutubishwa ili kubadilishana na kuongezwa kwa muda wa miezi mitatu wa kusitishwa kwa vikwazo, na kulitaja ombi hili kuwa halikubaliki.

"Wanataka tuwape uranium yetu yote iliyorutubishwa," Massoud Pezeshkian aliambia runinga ya serikali. "Baada ya miezi michache, watakuwa na mahitaji mapya," aliongeza.

"Kurejeshwa tena kwa maazimio yaliyobatilishwa hakuna msingi kisheria na hakuna uhalali, nchi zote lazima zijizuie kutambua hali hii haramu," wizara ya mambo ya nje ya Iran imesema katika taarifa yake leo Jumapili. "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itatetea kithabiti haki na maslahi yake ya kitaifa, na hatua yoyote inayolenga kudhoofisha haki na maslahi ya watu wake itakabiliwa na jibu thabiti na linalofaa," iliongeza.

Mwishoni mwa mwezi Agosti, Uingereza, Ufaransa, na Ujerumani zilianzisha utaratibu wa "snapback", ambao unaruhusu kurejeshwa kwa vikwazo vilivyoondolewa mnamo mwaka 2015 kufuatia makubaliano ya nyuklia ya Iran ndani ya siku 30. Kufuatia idhni ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kushindwa kwa Urusi na China mnamo Septemba 26 kuongeza muda huo, vikwazo vizito, kuanzia vikwazo vya silaha hadi hatua za kiuchumi, vimerejeshwa.
 

Vikwazo hivyo vinalenga makampuni, mashirika na watu binafsi wanaochangia moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja katika mpango wa nyuklia wa Iran au kutengeneza makombora ya balistiki, ama kwa kutoa vifaa vinavyohitajika, ujuzi au ufadhili.

Vikwazo hivyo ni pamoja na kuzuiliwa kwa silaha za kawaida, na kupiga marufuku uuzaji wowote au uwasilishwaji wa silaha kwa Iran. Uagizaji, usafirishaji au uwasilishwaji wa bidhaa na teknolojia zinazohusiana na mpango wa nyuklia na makombora ya balestiki utapigwa marufuku.

Mali ya mashirika na watu binafsi nje ya nchi ambazo ni mali ya watu wa Iran au makampuni yanayohusishwa na mipango ya nyuklia zitazuiwa. Watu walioteuliwa kushiriki katika shughuli zilizopigwa marufuku wanaweza kupigwa marufuku kusafiri ndani ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa. Nchi hizi wanachama pia zitalazimika kuzuia shughuli za benki na kifedha (utoaji wa huduma, ufadhili) ambazo zinaweza kusaidia Iran katika mipango yake ya nyuklia au makombora ya balestiki. Watu binafsi au makampuni yatakayokiuka masharti haya yatafungiwa mali zao kimataifa.