Kati ya fedha hizo, dola milioni 149.4 (sawa na shilingi bilioni 394.4) ni za kusaidia bajeti ya Serikali na kiasi cha dola milioni 786.2 (sawa na shilingi trilioni 2.07), ni za kugharamia mpango wa miezi 23 wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia dirisha la Resilient and Sustainable Fund (RSF).
Taarifa ya uamuzi huo uliofikiwa na Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika hilo imetolewa kupitia tovuti rasmi ya Shirika hilo, tarehe 20 Juni 2024, baada ya kumaliza mapitio ya tatu ya utekelezaji wa program ya Extended Credit Facility-(ECF), inayohusisha upatikanaji wa mkopo nafuu kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa nchi kupitia sekta za uzalishaji na huduma za jamii kwa Tanzania, ambapo mnamo Julai 2022, Shirika hilo lilidhinisha jumla ya dola za Marekani bilioni 1.1 (sawa na shilingi trilioni 2.4) kwa Tanzania.
Kukamilika kwa mapitio ya tatu ya Bodi hiyo, kumeruhusu Tanzania kupata mkopo nafuu wa dola za Marekani milioni 149.4 (sawa na shilingi bilioni 394.4), na kunakamilisha rasmi Tanzania kupata fedha zote ambazo ni takriban dola za Marekani milioni 606.4 chini ya Mpango wa ECF. Pia Shirika hilo, limeiongezea Tanzania miezi sita ya Utekelezaji wa Mpango huo wa ECF hadi Mei 2026, ili kutoa muda wa kutosha katika kutekeleza na kutimiza malengo makuu ya mpango huo.
Aidha, Shirika hilo limekubali ombi la Tanzania kupata fedha za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia dirisha la Resilient and Sustainable Fund (RSF) na kuipatia Tanzania mkopo huo nafuu wa kiasi cha dola za Marekani milioni 786.2 (Sawa na shilingi trilioni 2.07), ambazo zitasaidia juhudi za Tanzania katika kutekeleza Mageuzi ya Sera za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha ustahimilivu wa uchumi wake.
Mageuzi yatakayotokana na RSF, yanalenga kuimarisha uratibu wa sera za mabadiliko tabianchi, kuimarisha usimamizi wa namna ya kukabiliana na hatari za majanga, kuingiza sera za hali ya hewa kwenye mipango ya bajeti na uwekezaji, kuoanisha sera za sekta za hali ya hewa na sera za nchi, na kuimarisha uangalizi wa hatari zinazohusiana na mabadiliko ya tabianchi katika sekta ya fedha.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, ameishukuru IMF kwa uamuzi huo wa kuridhia maombi ya Serikali kuhusu mpango huo baada ya majadiliano ya kina na yenye manufaa kwa Tanzania, hatua ambayo amesema itasaidia kwa kiasi kikubwa kusaidia utekelezaji wa Bajeti Kuu ya Serikali kwa kuwekeza fedha hizo katika Sekta za uzalishaji pamoja na kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabianchi.
Ameahidi kuwa fedha hizo zitasimamiwa ipasavyo ili kukushukuru malengo ya upatikanaji wake kwa wanafunga ya wananchi na uchumi wa Taifa kwa ujumla.