Jumanne , 20th Jan , 2015

Ikulu imetoa tahadhari juu ya kuwepo kwa baadhi ya watu ambao ni matapeli na wanatumia vibaya jina la Ikulu kwa kudanganya kuwa Ikulu kuna nafasi za kazi na wana uwezo wa kuwapatia ajira hizo kwa masharti ya kutoa fedha.

Kurugenzi ya mawasiliano Ikulu jijini Dar es salaam nchini Tanzania imetoa tahadhari kwa wananchi juu ya kuwepo kwa baadhi ya watu ambao ni matapeli na wanatumia vibaya jina la ikulu kwa kusema kwamba kuna nafasi za ajira na wana uwezo wa kuwapatia ajira kwa kutoa fedha.

Tahadhari hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na Mkurugenzi wa mawasiliano Ikulu Bw. Salva Rweyemamu wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kufuatia kutokea kwa matukio kadhaa ya mfululizo ya watu kutapeliwa kwa kutafutiwa kazi ikulu.

Aidha Salva amesema Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kufanya maamuzi ya watuhumiwa wa kashfa ya Tegeta Escrow ambao walikuwa wakifanyiwa uchunguzi kama alivyoahidi wakati wa mkutano wake na wazee wa mkoa wa Dar es salaam tarehe 22 mwezi Disemba mwaka jana.