Alhamisi , 17th Dec , 2015

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bwana Jumanne Sagini amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati Mkoani Manyara Mhandisi Mussa Natty.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati ambaye kabla ya kuhamishiwa Wilayani Babati alikua Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni Jijini Dar es salaam Bw. Mussa Natty

Mhandisi Musa Natty ambaye kabla ya kuhamishiwa Wilayani Babati alikuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni Jijini Dar es salaam anatuhumiwa kwa ubadhirifu wa miradi mbalimbali ya wilaya ya Kinondoni.

Bw. Sagini amefafanua kuwa pamoja na kusimamishwa kazi, Mhandisi Natty anapaswa kurudi katika halmashauri ya manispaa ya Kinondoni na kusubiri uchunguzi zaidi dhidi ya tuhuma zinazomkabili.

Ametaja tuhuma hizo kuwa ni pamoja na usimamizi mbaya uliosababisha barabara za manispaa ya Kinondoni kujengwa chini ya kiwango na kutowachukulia hatua watendaji wa manispaa waliokuwa chini yake, ukosefu wa uadilifu katika ubinafsishaji wa eneo la ufukwe wa bahari la Cocobeach na malalamiko ya wananchi juu ya viwanja katika eneo la Kinondoni ulioambatana na usimamizi duni wa watumishi hasa wa sekta ya mipango miji na ardhi.