Jumanne , 7th Oct , 2014

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii nchini Tanzani imesema kuwa asilimia 0.7 ya Watanzania wote, ambao ni sawa na watu laki tatu na elfu kumi na tano wana tatizo la macho kiasi cha kutoona kabisa.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dk. Charles Pallangyo, amesema hayo leo wakati akizungumzia maadhimisho ya kimataifa ya siku ya macho ambayo nchini itafanyika Oktoba 9 mwaka huu.

Kwa mujibu wa Dkt Pallangyo, tatizo la upofu na uoni hafifu nchini hivi sasa linachangiwa na ongezeko la kasi la ugonjwa wa kisukari ambapo ameonya kuwa watu wanaougua kisukari wapo katika hatari kubwa zaidi ya kupata upofu.

Kwa upande wake, mratibu wa taifa wa huduma za macho kutoka wizara ya afya na ustawi wa jamii Dkt Nkundwe Mwakyusa, amesema kuwa wizara haina takwimu za idadi kamili ya watu wanaopata upofu kutokana na kuugua kisukari.

Dkt Mwakyusa amesema hali hiyo inatokana na kutokuwepo kwa huduma jumuishi ya kubaini upofu unaotokana na kisukari sambamba na uzembe wa baadhi ya wauguzi ya kutotaka kubaini magonjwa mengine yanayoambatana na kisukari.