Kutokana na kutokuwa na hospitali ya wilaya ya Namtumbo na Songea na hospitali ya halmashauri ya wilaya ya Songea hospitali ya rufaa ya mkoa wa Ruvuma imezidiwa kwa kufanya kazi zote zilizotakiwa kufanywa na hospitali hizo na hivyo baadhi ya wanawake wamekuwa wakipoteza maisha na watoto wao wakati wa kujifungua kutokana na kuzidiwa huko.
Hayo yamesemwa na mganga mfawidhi wa hospitali ya mkoa wa Ruvuma Dkt Benedict Ngaiza wakati alipoitwa na baraza la madiwani wa manispaa ya Songea kujibu hoja za malalamiko ya wananchi wanaolalamikia huduma za hospitali hiyo.
Daktari Ngaiza pia amejibu hoja mbalimbali za malalamiko ya wananchi yakiwemo ya kuombwa rushwa na ukosefu wa dawa ambapo amesema bajeti ya dawa katika hospitali hiyo ni milioni 750 kwa mwaka lakini imekuwa ikitengewa shilingi milioni 280 kwa mwaka.