Chama cha NCCR-Mageuzi kimeeleza kugundua mbinu chafu zinazopangwa na kikundi kinachotajwa kutaka kuwadhuru viongozi wa vyama vinavyounda Umoja wa katiba ya wananchi, UKAWA, hususan mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia.
Chama hicho pia kimesema kuwa hakitajiengua kwenye umoja huo kama inavyoelezwa na baadhi ya wanachama kwa madai ya umoja kushindwa kufikia baadhi ya makibaliano, hususan ya mgao wa majimbo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, mkuu wa kitengo cha sheria na hali za binadamu wa NCCR- Mageuzi Mohamed Tibanyendera amesema tayari wamefikisha taarifa hizo za kudhuru kituo cha polisi ambacho hata hivyo hawakukitaja.
Aidha, chama hicho kimeeleza kushangazwa na ujumbe kutoka ndani ya chama hicho uliozungumza na waandishi wa habari jana, ambapo kimesema kuwa makamu mwenyekiti wa chama hicho Leticia Mosorre aliyeongoza ujumbe huo vikao vyote vya UKAWA na anaelewa kila kitu.
Chama hicho kimewataka watanzania kuachana na nia ovu zinazolenga kuvuruga amani ya nchi, na kuwataka kuwa watulivu ili uchaguzi ufanyike kwa amani na kuainisha kuwa hakitavuruga muungano huo, na baada ya uchaguzi wataendelea kutatua baadhi ya changamoto.