Dkt. Selemani Jafo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).
Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam leo tarehe 27 Mei 2024; Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema kuelekea kilele cha Maadhimisho hayo tarehe 29 Mei , 2024, kutakuwa na uzinduzi wa shughuli mbalimbali zinazotekelezwa Chini ya mradi wa Urejeshaji wa Uoto wa asili.
Amesema mradi huo unatekelezwa katika Wilaya 7 kutoka kwenye Mikoa mitano ya Tanzania bara ambayo ni Iringa, Njombe, Mbeya, Rukwa na Katavi; hivyo kutakuwa na uzinduzi wa shughuli zinazotekelezwa na mradi huo Wilayani Mpimbwe Mkoani Katavi;
Shughuli zitakazozinduliwa ni Josho la Mifugo, Banio na Birika la Kunyweshea maji mifugo ambapo pia kutakuwa na shughuli za kugawa hati miliki za ardhi za kimila 4450 pamoja na hati ya Msitu.
Ameeleza kutakuwa na kongamano la Kitaifa la wadau wa Mazingira ambalo litakuwa na kauli mbiu isemayo "Mabadiliko ya Tabianchi na Athari zake"; kongamano hilo ambalo limeandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia Ofisi ya NEMC litafanyika tarehe 31 Mei, 2024 katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam.
Waziri Jafo amesema vilevile tarehe 1 Juni, 2024 kutakuwa na kampeni ya Usafi wa Mazingira Kitaifa ambayo itafanyika maeneo mbalimbali na kuanzia tarehe 1 hadi 6 Juni, 2024 kutakuwa na maonesho ya wiki ya Mazingira ambapo wadau mbalimbali watapata fursa ya kuonesha bidhaa, teknolojia, uvumbuzi na ubunifu wa masuala yanayohusu hifadhi ya uzimamizi wa Mazingira.
Maonesho hayo yanafanyika katika viwanja vya kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete Jijini Dodoma; ambapo uzinduzi wa maonesho hayo utafanyika tarehe 3 Juni, 2024 na mgeni Rasmi anatajiwa kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko.
Aidha Maadhimisho ya siku ya Mazingira Duniani 2024 yanaongozwa na kauli mbiu isemayo “Urejeshwaji wa Ardhi, Ustahimilivu wa hali ya Jangwa na ukame’’.