Jumatano , 13th Jul , 2016

Halmashauri za mikoa inayounda Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, zimetakiwa kukamilisha mchango wa shilingi milioni mbili kila moja kwaajili ya maandalizi ya maonesho ya wakulima ya Nanenane 2016 kabla ya Julai 19.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla

Agizo hilo limetolewa leo(Julai 13) na Mwenyekiti wa maandalizi hayo mkuu wa mkoa wa Mbeya Amos Makalla kwenye kikao kilichowakutanisha wajumbe mbalimbali kutoka halmashauri zote za mikoa ya kanda hiyo.

Makalla amesema kusuasua katika utoaji wa michango ya halmashauri kunaweza kuzorotesha maandalizi na kusababisha maonesho ya mwaka huu kukosa uzito unaostahili.

Amesema ni lazima makatibu tawala wa wilaya wahakikishe wanazibana halmashauri zote ili ziwasilishe michango kwa wakati na kuwezesha sekretarieti kuendelea na maandalizi na kuyakamilisha ndani ya muda uliosalia.

Akizungumzia adha ya uhaba wa maji unaokwamisha shughuli za umwagiliaji mimea kwenye vipando katika viwanja vya maonesho, Makalla aliiagiza Mamlaka ya Maji safi na usafi wa mazingira Mbeya (Mbeyauwusa) kuhakikisha maji yanapatikana wakati wote kwenye viwanja hivyo mpaka siku ya ukomo wa maonesho.

Katika kikao hicho baadhi ya wajumbe akiwemo Mkuu wa wilaya ya Iringa,Richard Kasesela wameitaka sekretarieti ya maandalizi kuyashirikisha makampuni makubwa yanayoweka mabango kwenye maeneo mbalimbali katika uwanja wa maonesho kuchangia gharama za maandalizi badala ya kuishia kulipa ada ya ushiriki wa maonesho pekee.

Kasesela amesema yapo makampuni ambayo yamediriki hata kuipa mitaa ndani ya viwanja hivyo majina ya bidhaa zao lakini hakuna mapato yoyote yanayotokana na matangazo hayo.