Alhamisi , 17th Jan , 2019

Wengi miongoni mwa wananchi wa mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma bado wanaendelea kudai malipo yao ya mauzo ya zao la Korosho walizouza msimu uliopita kwa serikali.

Korosho

Mara nyingi malipo ya mkupuo ya zao hilo kwa wakulima yamekuwa hayavuki zaidi ya mwezi wa kwanza ya kila mwaka, hilo limethibitishwa pia na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipokuwa akizungumza na Wakuu wa Mikoa hiyo inayozalisha Korosho kwa wingi, jana, Jumatano, Januari 16.

Katika kikao hicho cha Wakuu wa Mikoa pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo TADB alichokiendesha kwa njia ya video (video conferencing) kutokea ofisini kwake Mlimwa, Dodoma, Majaliwa amesema kwa kawaida ya malipo ya mkupuo kwa wakulima huwa yanakamilika ifikapo Januari 10 ya kila mwaka.

Hakikisha mnaharakisha malipo ya wakulima lakini pia suala la uhakiki linabaki palepale ili tuwalipe wakulima wanaostahili”, amemweleza Mkurugenzi Mkuu wa TADB, Bw. Japhet Justine.

Hili zoezi la uhakiki na malipo, lilianza Novemba 27, 2018 na leo ni tarehe 16 Januari, 2019 na hatujafika hata asilimia 50, maana yake zoezi hili tutalimaliza Aprili mwanzoni. Haiwezekani! Tunapata lawama kutoka kwa wakulima wa korosho kwa sababu hii kasi ni ndogo, na haya siyo malengo ya Mheshimiwa Rais, aliyetaka korosho zinunuliwe na Serikali”.

Baadhi ya wakulima wamekuwa wakilalamika kushindwa kuwapeleka shule watoto wao, wakisema sababu ni kutolipwa pesa zao, hali ambayo ilipelekea hadi Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba, Sebastian Waryuba kupiga marufuku wananchi kutumia kigezo hicho kutowapeleka watoto wao shule. 

"Tukiendekeza vitu kama hivi, jamii yetu itazidi kuwa duni na itadidimia kabisa, wazazi wanataka kupata kisingizio fulani ili wasiwapeleke watoto wao shule, eti kwasababu hatujalipwa fedha za korosho wakati mheshimiwa Rais ametoa elimu bure", alisema Mkuu huyo wa Wilaya.

Mkurugenzi Mkuu wa TADB, amesema kuwa fedha iliyolipwa kwa wakulima wa korosho hadi sasa ni sh. bilioni 306 kwa wakulima zaidi ya 156,000, na zaidi ya sh. bilioni 11 zikiwa zimekwama kulipwa kwani taarifa za kibenki zinaonyesha kuna matatizo hasa kwenye majina.

Bonyeza hapa chini kutazama zaidi.