Jumanne , 30th Jun , 2015

Waziri mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye leo amekuwa mwanachama wa 15 wa CCM kurudisha fomu yake ya kuomba kuteuliwa na chama chake kuwania nafasi ya Urais baada ya kukamilisha zoezi la kutafuta wadhamini mikoani.

Waziri mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye.

Sumaye amesema kuwa amejitathmini na kujiona kuwa anafaa kuwaongoza watanzania kwa kuwa yeye ni msafi kimaadili kiafya na kiutendaji kwa hiyo hana dosari yoyote katika kuwania nafasi hiyo.

Aidha amesema kuwa kipaumbele chake kikubwa kitakuwa katika kukuza uchumi kwa kuongeza uzalishaji na mauzo ya nje ya nchi ambapo amesema kwa kufanya hivyo ataweza kuuinua uchumi wa Taifa.

Amevitaja vipaumbele vingine kuwa ni pamoja na kuboresha huduma za kijamii ikiwa ni pamoja na kupambana na vitendo vya rushwa na ufisadi nchini.

Wakati huo huo mwanachama mwingine wa CCM Amon Siyantemi amerudisha fomu yake ya kuomba ridhaa ya kuwania urais kwa tiketi ya CCM na kusema kuwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini inatakiwa kuvunjwa kwani utendaji wake hauridhishi.

Amesema endapo atachaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ataunda chombo kingine cha kupambana na rushwa na kuivunja takukuru ili mishahara inayotumika kuwalipa wafanyakazi wa takukuru iende kuboresha huduma nyingine za kijamii kama vile afya na maji.

Jumla ya wawania urais nane kupitia CCM leo wanatarajiwa kurudisha fomu zao wakiwemo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Dk, Harrison Mwakyembe na Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa, Bernard Membe