Jumanne , 17th Feb , 2015

Mwenyekiti wa Baraza la ushauri la watumiaji wa huduma zinazodhibitiwa na Ewura, Profesa Jamidu Katima amewataka watumiaji wa nishati na maji nchini kufikisha malalamiko yao kuhusiana na huduma zinazotolewa na ewura ili ziweze kutafutiwa ufumbuzi.

Mwenyekiti wa Baraza la ushauri la watumiaji wa huduma zinazodhibitiwa na Ewura, Profesa Jamidu Katima

Profesa Katima ametoa kauli hiyo leo mjini Dodoma kwenye mkutano wa kwanza wa mwaka wa Baraza la ushauri la watumiaji wa huduma zinazodhibitiwa na Ewura (RCC- EWURA) mjini Dodoma.

Amesema kumekuwa na tabia ya watumiaji wa huduma zinazotolewa na Ewura kupelekewa ankara kubwa za huduma wanazotumia kuliko matumizi yao lakini wanaishia kunung’unika bila kuyafikisha malalamiko hayo kwenye mamlaka husika.

Aidha amewataka wateja wa huduma zinazodhibitiwa na Ewura kutumia huduma hizo kwa uangalifu ili waweze kulipa gharama sawa na huduma walizozitumia.

Kwa upande wake mwenyekiti wa RCC ya Rukwa, Faustina Valeri amesema kuwa changamoto kubwa wanayokabiliana nayo katika shughuli zao za kila siku ni uelewa mdogo wa wananchi kuhusiana na kazi za baraza hilo na hivyo kutaka elimu zaidi itolewe kwa wananchi kuhusiana na kazi za baraza hilo.