Jumanne , 19th Sep , 2023

Viongozi pamoja na wananchi wilayani Kilwa wametakiwa kujitathmini endapo Serikali itaendelea kuweka juhudi kubwa kwa kutoa Fedha kwaajili ya miradi ya maendeleo na hali ya wananchi kubaki kuwa duni. 

Rais Samia Suluhu Hassan

Maneno hayo yamesemwa na Rais Samia Suluhu Hassan akiwa katika mkutano na wananchi baada ya kufanya zoezi la kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa bandari ya uvuvi na kugawa boti za kisasa kwa wavuvi na wanawake wilayani Kilwa.

"Kilwa isipobadilika naomba mukae kitako mjiulize kwanini, kwa serikali tunajitahidi kuleta fedha, fedha zinaletwa kuwasaidia wananchi na sio viongozi kujinufaisha," amesema Rais Samia

Rais Samia amesema, kwa historia kubwa ya Mji wa Kilwa wananchi wake hawakupaswa kuwa wanyonge, serikali imedhamiria kuwainua wananchi hao kiuchumi kwa kupeleka miradi mingi na mikubwa huku akiwaonya viongozi mkoani humo kutotumia pesa za miradi vibaya kwani dhamira kuu ya pesa hizo ni kuwanufaisha wananchi.

Katika ziara yake Kilwa Masoko, Rais Samia ameweka Jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa bandari kubwa ya uvuvi inayokadiriwa kumalizika ndani ya miezi 36 (miezi 24 ujenzi, mwaka mmoja uangalizi) huku kiasi cha fedha shilingi bilioni 280 zikitajwa kutengwa kwa ajili ya mradi huo.

Aidha, Rais Samia amekabidhi boti 160 zitakazotumika kwa ajili ya shughuli za uvuvi na kuwasaidia wakulima wa Mwani Baharini ambapo boti hizo zimetolewa kwa mkopo nafuu kwa wananchi wa Pwani, Lindi na Mtwara na zinatajwa kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya uvuvi kwani zina ukubwa wa kutosha wa kubeba samaki na zinauwezo wa kusafiri kwenda masafa marefu baharini.