Jumanne , 5th Jul , 2016

Baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani wameeleza masikitiko yao juu ya kuondoka kwa aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Mtwara Bi. Fatma Ally, ambaye ni miongoni mwa wakuu wa wilaya ambao hawakuteuliwa tena katika uteuzi mpya uliofanywa na rais.

Aliekua Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Fatma Ally aliesimama akiongea katika moja Mikutano yake na Wananchi (Kushoto) ni Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Halima Dendego.

Wakizungumza baada ya hafla fupi ya kukabidhi ofisi kwa Mkuu wa wilaya mpya Dkt. Khatibu Kazungu, wamesema Fatma alikuwa na mahusiano mazuri na jamii na kwamba miongoni mwa mambo yatakayokumbukwa ni wepesi wake katika kusuluhisha migogoro mbalimbali inayowahusu wananchi wake.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Bi. Fatma amesema katika uongozi wake amesaidia kuirejesha amani ya Mtwara ambayo wakati anaanza kazi haikuwa rahisi kwa kiasi kikubwa pamoja na kupunguza kasi ya uvuvi haramu, huku mkuu wa wilaya hiyo Dkt. Kazungu akiwataka wananchi na viongozi wenzake kushikamana katika kazi ili kufanikisha maendeleo.

Fatma ambaye kabla ya kuhamishiwa wilaya ya Mtwara aliwahi kuongoza wilaya za Nanyumbu mkoani humo na Chamwino mkoani Dodoma, amekabidhi michango ambayo alifanikiwa kuikusanya kutoka kwa wananchi kupitia kampeni yake ya Haba na Haba katika kutatua uhaba wa madawati ambayo ni fedha kiasi cha shilingi milioni ishirini na tano laki tano na elfu ishirini na moja, huku wilaya ikiwa imekamilisha tatizo la madawati kwa asilimia 100.