Jumanne , 1st Mar , 2016

Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji nchini (EPZA), imejipanga kuzalisha bidhaa zenye viwango vya kimataifa ili kuendeleza kukuza soko la nje kwa bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi kwa kupitia rasimali za hapa nchini.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji nchini (EPZA), Luteni Joseph Simbakalia

Akizungumza jana Jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo Luteni Joseph Simbakalia amesema kuwa ili kukuza uchumi wa nchi wamepanga kuunganisha sekta hiyo na wizara tofauti ambazo zinazalisha vitu mbalimbali ikiwemo sekta ya mifugo kwa kutumia ngozi ambayo inaweza kutumika kutengenezea viatu.

Aidha mkurugenzi huyo ameongeza kuwa katika siku za mbeleni amedhamiria kutungeneza viwanda vikubwa ikiwemo vya kuunganisha au kutengeneza magari, Mabehewa ya treni na bidhaa zingine za chuma mara baada ya uzalishaji wa chuma wa liganga kuimarika.

Ameongeza kuwa wanalenga zaidi kuuza nje ingawa hata ndani bidhaa hizo zitapatikana na kusema lengo la kuuza sana nje ni kuweza kupanua zaidi sekta ya viwanda nchini ambayo ndiyo chachu ya uchumi wa nchi kwa serikali ya awamu ya tano.