Alhamisi , 24th Sep , 2015

Serikali imetakiwa kutoa elimu ya kina kwa vijana juu ya mikopo inayotolewa na serikali, ili kuwaelimisha vijana na kuwafanya watambue haki zao juu ya mikopo hiyo.

Wito huo umetolewa na Bi. Hanifa Chiwili alipokuwa akiongea kwenye kipindi cha Super Mix kinachorushwa na East Africa Radio, kuhusu nini serikali ijayo ifanye ili kuboresha mikopo kwa vijana.

Bi. Hanifa amesema vijana wengi sasa hivi hawajui njia za kuweza kupata mikopo hiyo ambayo inatoka serikalini na kupitia serikali za mitaa, na matokeo yake kujikuta wanaingia kwenye madhila mbalimbali baada ya kuomba pesa kwenye taasisi binafsi za kifedha.

"Vijana wa sasa wanapata madhila wanapoenda kutafuta mikopo, mingi imekuwa ya kibiashara kwa sababu hawajui njia ya kufika kwenye mikopo ya serikali kwa sababu inapitia serikali za mitaa au halmashauri, kwa hiyo serikali isimame kuwaelimisha vijana kuwafanya watambue haki zao juu ya mikopo hii". alisema Bi. Hanifa.

Pia Hanifa ameitaka serikali kulegeza masharti ya mikopo hiyo, kwani mingi inakuwa na masharti magumu ambayo vijana wanashindwa kuyatimiza na kusababisha kukosa sifa za kupata mikopo hiyo.

"Serikali iangalie mikopo inayotoka ni ya namna gani, walegeze masharti ya dhamana, unakuta mikopo inataka uwe una miliki ardhi na tunajua vijana wengi hawamiliki ardhi, matokeo yake wananaenda kwenye taasisi nyingine ambazo huko nako wanakutana na riba kubwa", alisema hanifa.

Pamoja na hayo Bi Hanifa pia amewataka vijana kuhudhuria kwenye mikutano ya kampeni ili waweze kuwahoji wagombea wao juu ya matakwa yao, na kutaka kuendelea kuifuatilia serikali kwa kile wanachokifanya na kusimama imara.