Ijumaa , 22nd Aug , 2014

Ujumbe wa Tume ya Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki leo umetembelea vyombo vya habari vilivyo chini ya makampuni ya IPP na kuelezea kuridhishwa na umahiri pamoja na teknolojia ya kisasa inayotumiwa na vyombo hivyo katika uandaaji wa habari.

Wajumbe wa Tume ya Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki wakiongozwa na Spika wa Bunge hilo Bi. Margareth Ziwa walipotembelea vyombo vya habari vinavyomilikiwa na makampuni ya IPP.

Ujumbe huo umeongozwa na Spika wa Bunge la Afrika Mashariki Bi. Magreth Zziwa na kupata fursa ya kutembelea vyombo hivyo ambavyo ni East Africa Television – EATV, East Africa Radio, Capital TV, Capital Radio, ITV, Radio One, pamoja na kampuni ya magazeti ya The Guardian LTD ambayo huchapisha magazeti ya The Guardian, Nipashe pamoja na gazeti la Sema Usikike.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa wawakilishi wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki Alhaj Adam Kimbisa amesema ziara ya ujumbe huo wameifanya wakati bunge hilo likijiandaa na vikao vyake vitakavyoanza mapema wiki ijayo katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam.

Kimbisa amesema kufanyika kwa vikao vya bunge hilo jijini Dar es Salaam, kuna umuhimu mkubwa hivi sasa ambapo kumekuwa na juhudi mbalimbali za kuimarisha ustawi wa maisha ya wakazi wa Afrika Mashariki, hasa kupitia uondoaji vikwazo visivyo vya kiforodha vinavyosababisha kupanda kwa bei za bidhaa na ugumu wa maisha.