Jumanne , 12th Jan , 2016

Leo ni sikukuu ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo wazanzibar wanasheherekea miaka 52 ya Mapinduzi ya Januari 12 mwaka 1964, ambayo yaling’oa utawala wa Sultani kutoka Oman na kuwezesha wazalendo wengi kushika hatamu ya kuongoza nchi.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein anatarajiwa kuhutubia maelfu ya wananchi ambao wamehudhuria katika uwanja wa Amaan.

Atapokea maandamano ya wananchi wa mikoa mitano ya Unguja. Matukio mengine makubwa yatakayofanyika katika uwanja huo ni Rais Shein kukagua gwaride la heshima la vikosi ya ulinzi na usalama, vikiongozwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) .

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na idara ya sherehe na mapambo iliyo chini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, sherehe hizo zitahudhuriwa na viongozi wa ngazi za kitaifa akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano, John Magufuli ambaye ni mara ya kwanza kushiriki baada ya kuchaguliwa katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 mwaka jana.

Aidha Ratiba hiyo inaonesha kwamba sherehe hizo, zitahudhuriwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na marais wastaafu wa Jamhuri ya Muungano na wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.