Alhamisi , 30th Nov , 2023

Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) Dkt. Tulia Ackson, ameielekeza kamati inayoshughulikia masuala ya Mashariki ya Kati ya Umoja huo kutembelea Israel na Palestina mapema katika juhudi za kutafuta suluhusho inayoweza kuhakikisha amani na usalama vinapatikana kufuatia mgogoro unaoendelea

Dkt Tulia alipotembelea kwenye moja ya maeneo yaliyoathirika kutokana na mzozo wa Israel na Palestina

Dkt. Tulia ameyasema hayo leo tarehe 30 Novemba, 2023 Jijini TelAviv nchini Israel mara baada ya kumaliza ziara yake ya kikazi ya siku mbili iliyompa fursa ya kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali wa Israel na mamlaka ya Palestina.

"Nimekuja kutembelea maeneo ya Palestina na Israel ambao wote hawa mabunge yao ni wanachama wa IPU lakini muhimu zaidi kuwafahamisha kuwa tupo pamoja nao katika kipindi hiki kigumu na kamati yetu inayoshughulikia masuala ya Mashariki ya Kati itakuwa hapa siku zijazo kutafuta uhalisia wa mgogoro huu na kuleta taarifa ambayo tutapata nafasi ya kuijadili ili tuone huko mbele tunakokwenda tunawezaje kuwa na amani na usalama kwa watu wote," amesema Dkt. Tulia

Amefafanua kuwa, moja ya msingi wa IPU ni kuhakikisha uhai wa kila binadamu unalindwa na Umoja huo utafanya kila linalowezekana ili dunia iwe sehemu salama na ya amani kwa binadamu wote bila kujali rangi, itikadi, imani na maeneo wanayotoka.