Jumatano , 16th Nov , 2016

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein ametia saini Muswada wa Sheria ya Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia ya mwaka 2016, na kusisitiza wananchi kufaidika kupitia mkataba huo.

Dkt. Shein akisaini sheria hiyo

 

Akizungumza mara baada kusaini sheria hiyo aliwaeleza viongozi na waandishi wa habari kuwa sheria hiyo namba 6 ya mwaka 2016 inaipa Zaznzibar mamlaka ya kisheria ya kuendeleza rasilimali ya mafuta na gesi ambapo kabla ya hapo sheria hiyo haikuwepo.

Dkt. Shein alisema kitendo cha kutia saini sheria hiyo hakijavunja katiba ya jamhuri ya muungano kama baadhi ya watu wanavyodai na kuwataka kusoma sheria ya mafuta namba 21 ya mwaka 2015 iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kuhusu mapato yatokanayo na shughuli hizo za mafuta na gesi Dkt. Shein Alieleza kuwa sheria hiyo inatamka kuwa kwa upande wa Tanzania Bara mapato yatatumiwa na serikali ya Jamhuri ya muungano kwa faida ya Tanzania Bara na kwa upande wa Zanzibar mapato hayo yatatumiwa na serikali ya mapinduzi ya Zanzibar kwa faida ya Zanzibar.