Alhamisi , 27th Mei , 2021

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, amezitaka kampuni zote zinazoagiza mbegu kutoka nje ya nchi kuanza kuzalisha mbegu hizo hapa nchini huku akiagiza Wizara ya Kilimo ijipange kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa agizo hilo.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango

Dkt. Mpango ametoa maagizo hayo hii leo wakati akihutubia katika Maadhimisho ya Kumbukizi ya Hayati Edward Moringe Sokoine yaliyofanyika katika Chuo cha Kilimo cha Sokoine (SUA) ambapo amesema nchi haiwezi kuwa nchi ya kipato cha kati cha juu kama mienendo yetu si ya tija.

“Nichukue nafasi hii kuzitaka kampuni zote ambazo zinaagiza mbegu kutoka nje zizalishe mbegu hizo hapa nchini na Wizara ya kilimo ijipange kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa maagizo haya, wasisubiri nitakapowauliza,” amesema Dkt. Mpango.

Awali akielezea Juu ya Hayati Edward Moringe Sokoine amesema aikuwa kiongozi mzalendo na aliyejitoa kushughulikia masuala ya kilimo, uvuvi na ufugaji.

“Hayati Sokoine alijitoa sana kwa maendeleo ya uvuvi, kilimo na ufugaji nchini alijitoa sana kuanzishwa kwa chuo cha SUA, chuo hiki kinachosababu ya kumuenzi, sio wengi wanatambua kuwa kilimo ni Sayanasi lakini Hayati Sokoine alikuwa kati ya viongozi waliotambua umuhimu wa kilimo kwamba ni Sayansi nakuweka msisitizo kwenye tafiti na kutengeneza wataalum wa kilimo,” amesema Dkt. Mpango.

Sambamba na hilo Dkt. Mpango aliafikiana na ombi la familia ya Hayati Sokoine juu ya kuandaliwa kitabu cha Kiongozi huyo juu ya mchango wake kitaifa na Chuo cha SUA.
 
Katika maadhimisho hayo ambayo yanaamabatana na mdahalo wa kitaifa ya Kumbukizi ya Hayati Edward Moringe Sokoine yamehitimishwa leo na Dkt. Mapngo ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi.