Jumanne , 6th Dec , 2022

Watu 14 akiwemo Diwani wa Kata ya Buzilasoga David Shilinde, Mwenyekiti wa CCM Kijiji cha Ikoni B William Nengo na Afisa Mtendaji wa Kijiji hicho Tiluloza Alphonce, wamefikishwa katika mahakama ya wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza kwa tuhuma za mauaji ya mwanamke aitwaye Getruda Dotto.

Diwani na wenzake 13 walivyofikishwa mahakamani

Ni kesi namba 23 ya mwaka 2022 ambayo leo hii imetajwa katika Mahakama ya wilaya ya Sengerema mbele ya Hakimu Mfawidhi Tumsifu Barnabas, ambapo Mwendesha Mashtaka wa serikali Theophilius Lucas, ameiambia Mahakama hiyo kuwa upelelezi wake bado haujakamilika na kuomba ipangiwe tarehe nyingine.

Baada ya maelezo hayo ya Mwendesha Mashtaka Hakimu Tumsifu Barnabas, akaiahirisha kesi hiyo hadi Desemba 20 ya mwaka huu huku washtakiwa wakirudishwa rumande katika gereza la Kasungamile.

Inadaiwa kuwa mnamo Novemba 5, 2022, majira ya saa 2:00 asubuhi katika Kitongoji cha Ikoni B, Kata ya Buzilasoga wilayani Sengerema mwanamke huyo aliyejulikana kwa jina la Getruda Dotto akiwa nyumbani kwake na watoto wake wawili ghafla alivamiwa na kundi la watu wakiwemo viongozi hao wakaanza kumshambulia kwa kutumia fimbo na marungu huku wakimtuhumu kuiba mihogo kwenye shamba la mwanakijiji mwenzake.

Inaelezwa kuwa mwanamke huyo alijaribu kujiteteana kusema shamba hilo aliachiwa na marehemu mume wake  lakini watu hao waliendelea kumshambulia na baadae wakamchoma moto na kupelekea kifo chake.