Jumatano , 26th Oct , 2016

Mkuu wa wilaya ya Arumeru Alexander Mnyeti, amewaagiza watendaji wa serikali katika ngazi za vijiji, kata na tarafa kurejesha adhabu za viboko katika maeneo yao kwa watu wanaokunywa pombe muda wa kufanya kazi.

Mkuu wa wilaya ya Arumeru Alexander Mnyeti

 

Mnyeti ametoa agizo hilo jana katika kikao kilichowashirikisha wenyeviti wa vijiji,watendaji wa Vijiji,Kata na Tarafa wa wilaya ya Arumeru mkoani hapa.

Amesema watendaji hao wana wajibu wa kuhakikisha kuwa muda wa kazi hakuna mtu anayekunywa pombe katika maeneo yao kwani kumekuwa na tabia yaa baadhi ya watu hasa vijana kunywa pombe kuanzia asubuhi.

Aidha amesema kuwa akikuta watu wanakunywa pombe muda wa kazi atawawajibisha watendaji wa eneo husika, kwani shughuli za maendeleo zinashindwa kufanyika kutokana na vijana wengi kushindwa kufanya kazi kwa sababu ya ulevi.

Alexander Mnyeti siku aliyokula kiapo kuwa Mkuu wa wilaya ya Arumeru

 

Pia amewapa siku 21 wakurugenzi wa halmashauri za Meru na Arusha Vijijini zilizopo wilayani humo, kuhakikisha kuwa wanahamisha ofisi za serikali za vijiji na kata zilizopo katika majengo yanayomilikiwa na CCM.

Amesema  wakurugenzi hao watafute ofisi nyingine za kupanga au wajenge katika vijiji hivyo, kwani kumekuwa na malalamiko mengi kuhusiana na ofisi hizo zinazomilikiwa na CCM ambapo wakati mwingine wakishinda wapinzani katika baadhi ya maeneo hayo, wanadai ofisi hizo ni za umma wakati zinamilikiwa na CCM.