Jumanne , 1st Jul , 2014

Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia nchini Tanzania COSTECH inatekeleza miradi kadhaa inayolenga kupunguza kiwango cha umaskini na tatizo la ajira kwa vijana, hususani wale wanaohitimu katika fani za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.

Mkurugenzi wa tume ya taifa ya sayansi na teknolojia Dkt Hassan Mshinda.

Mratibu wa mfuko wa taifa wa uendelezaji wa sayansi na teknolojia kutoka COSTECH Dkt Bakari Msangi, amesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akifafanua kuhusu nafasi ya watafiti na wanasayansi katika kukabiliana na kero mbali mbali zinazoikabili jamii.

Dkt Bakari ameitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na ule wa hatamizi ambapo wahitimu wa masomo ya sayansi hupewa maarifa na ujuzi wa kisayansi wa namna ya kubuni miradi itakayozalisha ajira kwa watu wengi, kuongeza kipato huku ikisaidia kutatua kero mbali mbali katika jamii.

Mbali ya mradi wa hatamizi, Dkt Msangi amesema COSTECH pia imefanya utafiti na kufanikiwa kuja na mbegu bora za mazao ikiwemo mbegu mpya ya mpunga ambapo mkulima kutumia kilo tatu tu badala ya kilo kumi za mbegu kwa kila hekta moja anayolima, huku akipata takribani tani saba za mpunga kutoka mavuno ya tani mbili kwa kila hekta.

Mradi mwingine kwa mujibu wa Dkt Msangi ni ule wa utafiti uliosaidia kupatikana kwa chanjo tatu mpya kwa ajili ya kuzuia ugonjwa wa mdondo ambao kwa kiasi kikubwa unawashambulia mifugo jamii ya kuku.

Dkt Msangi amesema hivi sasa serikali inaendelea na mazungumzo na serikali ya Morocco kwa ajili ya kuanza kuzalisha, kuuza na kusambaza chanjo hiyo ambayo amesema kupatikana kwake kunaiweka Tanzania katika fursa nzuri ya kunufaika kiuchumi lakini pia kuongeza juhudi za kuutokomeza ugonjwa wa mdondo.

Dkt Msangi amewataka vijana kutumia matokeo ya tafiti mbali mbali za kisayansi zilizofanywa na COSTECH, ili kubuni miradi itakayowasaidia kutengeneza ajira, badala ya kukaa vijiweni wakitegemea ajira za maofisini ambazo amesema kuwa ni chache na haziwiani na ukubwa wa idadi wahitimu kutoka vyuo vya elimu ya juu nchini.
-----------------------------------