Jumatatu , 30th Jun , 2014

Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia COSTECH imewataka wasomi watafiti nchini kufanya tafiti za jinsi teknolojia inavyoweza kutumika katika kupunguza umaskini hususani jinsi ukuaji wa uchumi unavyoweza kuwa na maana katika pato la mtu mmoja mmoja.

Mkurugenzi mkuu wa tume ya taifa ya sayansi na teknolojia COSTECH Dkt Hassan Mshinda (kulia) akiwa katika moja ya mikutano ya kujadili ukuaji wa sekta ya sayansi na teknolojia.

Akiongea leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo, Dkt. Hassan Mshinda amesema wanasayansi na wanazuoni kupitia taasisi yao ya STIPRO wafanye utafiti wa teknolojia ya simu za mkononi zinavyoweza kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii sambamba na kupendekeza kiwango halisi cha pesa kinachotakiwa kutengwa katoka pato la taifa kwa ajili ya shughuli za utafiti.

Dkt Mshinda alikuwa akizungumza kwenye mkutano wa wadau na wanachama wa STIPRO ambao wanakutana kwa ajii ya kujadili mpango mkakati wa miaka mitano wa taasisi hiyo ambao unalenga kuona ni kwa namna gani taasisi hiyo itashughulikia tafiti na sera za sayansi na teknolojia kwa ajili ya kuishauri vema serikali kwenye eneo hilo.

Kwa mujibu wa Dkt Mshinda, matatizo yanayoikabili Tanzania kwa sasa yanahitaji suluhu za kisayansi na kwamba ni wakati muafaka kwa watafiti na wanasayansi kufanya utafiti lakini pia kuvishauri vyombo vya maamuzi juu ya teknolojia na tafiti walizozifanya ambazo wanadhani zitaongeza kasi ya kukabiliana na changamoto za kiuchumi na kijamii.

Kwa upande wake, mkurugenzi mtendaji wa STIPRO Dkt Bitrina Diyamett amesema kwa kiasi kikubwa mawazo yaliyotokana nautafiti wa taasisi hiyo yametumika katika kuandaa mpango wa kitaifa wa kuendeleza shughuli za utafiti na ubunifu wa kisayansi pamoja na uandaaji wa mpango wa maendeleo wa umoja wa mataifa ujulikanao kama Post 2015 Development Agenda, mpango mpya wa maendeleo utakaotekelezwa baada ya kukamilika kwa mpango wa maendeleo wa millenia hapo mwakani.