Ijumaa , 29th Sep , 2017

Ikiwa leo ni siku ya maadhimisho ya moyo duniani, Dkt. Emmanuel Bwana mtaalamu wa magonjwa ya moyo amesema vijana wengi wa sasa wapo katika hatari ya kupata ugonjwa huo kutokana na matumizi mengi ya Chumvi yasiyokuwa ya ulazima.

Dkt. Emmanuel amebainisha hayo kupitia kipindi cha East Africa Breakfast kutoka East Africa Radio na kuwataka waache matumizi hayo yasiyokuwa ya lazima katika utumiaji wa chumvi ambayo haijapikwa katika vyakula vyao pindi wanapokula.

"Ulaji wa chumvi kwa watu wengi umekuwa ni mkubwa, kulingana na tafiti nyingi zilizofanywa na madaktari bingwa wengi tokea mwaka 2014 mpaka sasa zinaendelea nyingine ni kweli inaonesha kwamba vijana wengi wapo katika hatari ya kupata magonjwa ya moyo, lakini pamoja na hayo hata matumizi ya pombe yamekuwa makubwa sana kipindi hiki kwa hiyo nayo inachangia ongezeko la magonjwa ya moyo", amesema Dkt.Emmanuel

Pamoja na hayo, Dkt.Emmanuel ameendelea kwa kusema "Vijana wa sasa hivi wamekuwa 'busy' kupita kiasi na kufanya na hata vile vyakula wanavyokula havina mfumo mzuri wa lishe ambayo ni sahihi ya kulinda afya zao. Kwa hiyo unakuta wanamrundikano wa mafuta katika miili yao ambayo hayana afya nzuri katika moyo".

Msikilize hapa chini Dkt. Emmanuel Bwana mtaalamu wa magonjwa ya moyo akielezea sababu za vijana wengi wa sasa kuwa na matatizo ya moyo.