Jumamosi , 1st Jul , 2023

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali haitoruhusu wafanyabiashara wa kanda ya kaskazini wanaokwenda kuchukua mafuta kwenye bandari ya Dar es salaam na badala yake imeagiza wafanyabiashara hao kuchukua bidhaa hiyo katika bohari ya mafuta iliyopo jijini Tanga

Pia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Nishati iratibu ununuzi wa mafuta kutoka mikoa ya Kaskazini na Kanda ya Ziwa ili yachukuliwe kutokea Tanga badala ya Dar es Salaam.

Kauli hiyo imetolewa na waziri Mkuu Kassim Majaliwa  wakati wa ziara yake ya siku moja jijini Tanga mara baada ya kutembelea bohari ya mafuta ya GBP. 

"Mikoa ya Mara, Mwanza, Manyara, Arusha, Kilimanjaro inafuata mafuta Dar es Salaam sababu ya mazoea lakini upatikanaji rahisi ni hapa Tanga, upatikanaji wa haraka sababu ya teknolojia ni hapa Tanga. Wizara ya Nishati watekeleze maelekezo haya ili wauzaji wa mafuta wayafuate Tanga," amesema.

Waziri Mkuu amesema endapo makampuni yote ya mikoa ya Kaskazini yatachukulia mafuta Tanga, uchumi wa mkoa huo utakua kwa haraka.

Akielezea kuhusu uwekezaji kwenye bohari hiyo, Waziri Mkuu amesema uwekezaji uliofanyika ni mkubwa kwani matenki yaliyopo yanaweza kupokea mafuta moja kwa moja kutoka bandarini na kuhifadhi lita hadi milioni 200.
 “Huu ni mkakati wa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kuendeleza uchumi wa nchi yetu. Wakati Serikali inaongeza uwezo wa kusimamisha meli zaidi bandarini, tutahakikisha kuwa uwekezaji huu unaleta faida kwa mwekezaji na unaongeza ajira kwa wanaTanga,” amesema

Mapema, akitoa taarifa kuhusu bohari hiyo ya GBP, Mkurugenzi Mtendaji wa GBP Badar Sood alisema ujenzi wa matenki hayo ulianza mwaka 2002 yakiwa na uwezo wa kuhifadhi lita milioni 25 huku wakipokea meli zenye uwezo wa lita 6,000 tu.

Akiwa katika bohari hiyo waziri Mkuu amekutana na kero ya wafanyabiashara kuchukulia mafuta jijini Daresalaam badala ya kuchukulia bidhaa hiyo kwenye bohari ya Tanga. 

Akiwa kwenye bandari ya Tanga, Waziri Mkuu alipokea taarifa ya uboreshaji wa miundombinu na kuelezwa kuwa ujenzi wa gati mpya umekamilika kwa asilimia 99 na kwamba zimebakia kazi ndogo za kukamilisha mifumo ya umeme.

“Uboreshaji wa bandari ya Tanga hadi sasa umegharimu sh. bilioni 429.2. Awamu ya kwanza ulihusisha uchimbaji wa eneo la kuingilia meli na kugeuzia lenye urefu wa km.1.7 na upana wa mita 75 kwa kina cha mita 10 na awamu ya pili ni kujenga gati yenye urefu wa mita 450,” alisema Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Juma Kijavaro.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa kwenye ziara yake ya siku moja Mkoani Tanga mbali na kutembelea kampuni ya GBP,  ametembelea uendelezaji wa bandari ya Tanga sambamba na kiwanda cha Maweni Lime stone ambapo alisikiliza kero za wawekezaji.