Mkataba huo umesainiwa Machi 16, 2023 kwenye kilele cha Maadhimisho ya Miaka 50 ya Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro yaliyofanyika kwenye Ofisi za Makao makuu ya Hifadhi ya Kilimanjaro.
Wakati wa utiaji saini mkataba huo Tanzania imewakilishwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Anderson Mutatembwa na Balozi wa China Mhe. Cheng Mingjian nchini ameiwakilisha nchi yake.
Pamoja na hayo Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa ambaye ndiye Mgeni Rasmi ameshuhudia tukio huku akimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan kwa kuifungua Tanzania duniani kupitia Mlima Kilimanjaro katika Filamu ya Royal Tour.
Ameongeza, Mlima Kilimanjaro unaopatikana nchini Tanzania ni nembo ya Afrika, kwani ndio mlima mrefu kuliko yote Afrika na kwamba Mlima huu pia ni mlima mkubwa duniani ambao upo huru kwa maana ya kwamba umesimama peke yake pasipo kuwepo kwa safu za milima kama ilivyo milima mingine duniani.