Akipokea msaada huo kwa niaba ya serikali; Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu amesema vitendo vya ugaidi sasa vimepata mwarobaini wake huku akiwataka wale wote wanaojishughulisha na ujangili kuacha mara moja.
Aidha ameongeza awali walikuwa wanakabiliwa na changamoto kubwa wa ukaguzi wa nyara katika makontena yanayoingia na kutoka kupitia bandari za Tanzania lakini kwa sasa wameshapata vifaa maalum vitakavyosaidia ukaguzi huo huku akiwaasa wanawake ambao imebainika kubobea katika usafirishaji wa nyara za maliasili kwa njia hiyo kuacha mara moja.
Kwa upande wake Balozi wa China hapa nchini Lu Youqing amesema Serikali yake ipo bega kwa bega na Tanzania katika kuwakomboa wananchi wake kiuchumi kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii ambayo imeleta mapinduzi makubwa katika kuongeza pato la Taifa ambapo wametoa msaada wa magari 50 yenye thamani ya shilingi bilioni 2.6.