
Akizungumza kwenye kipindi cha East Africa BreakFast cha East Africa Radio, mkurugenzi wa Idara ya Elimu wa asasi ya Pamoja 'Youth Organization' inayojihusisha na utetezi wa haki za watoto na vijana, mwalimu Gregory Paul amesema, tukio lililotokea mkoani Kagera linapaswa kuizundua serikali na ione umuhimu wa kusimamia vyema sheria na kanuni za viboko mashuleni lakini pia iweke walimu wa saikolojia wanaoweza kuwapa tiba ya kisaikolojia walimu na wanafunzi kama inavotakikana na sera ya elimu.
“Mwalimu huenda anakuwa na msongo wa mawazo hivyo anapokutana na mtoto amekosea anajikuta akitaka kumalizia hasira zake pale”, amesema Mwl. Gregory
Aidha ameongeza kuwa shule za serikali pia zimekuwa na tabia ya kutofatilia hali za wanafunzi na mara nyingi walimu wakuu wamekuwa wakihangaika na majukumu mengine wakijisahau kuzungumza na wanafunzi ili kujua changamoto zao hivyo watoto wanakosa haki ya kusikilizwa.
Agosti 27, mwanafunzi wa darasa la tano Siperius Eradius wa shule ya Msingi Kibeta, manispaa ya Bukoba mkoani Kagera aliadhibiwa na mwalimu wake Respicius Patrick kiasi cha kusababishiwa kifo, kutokana na kudaiwa kuiba mkoba wa mwalimu ambao baadaye ulipatikana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustino Ollomi amesema kuwa Patrick, ambaye ni mwalimu wa nidhamu anadaiwa kumpiga mwanafunzi huyo akihusishwa na upotevu wa mkoba wa mwalimu Herieth Gerard, uliokuwa na Shilingi elfu 75,000 na vitambulisho vyake tayari anashikiliwa na jeshi hilo huku uchunguzi zaidi ukiendelea kuhusiana na tukio hilo.