Mashine ya kisasa ya kujiandikisha kitambulisho cha kura.
Akizungumza na East Africa Radio msimamizi wa mashine za BVR, Astori Mgwame amesema kuwa wananchi hao waligomea mashine hizo kwa kuwa zilikua hazina muendeshaji wa kuziendesha kwa ufasaha na kusema kuwa hawatajiandikisha mpaka wahakikishiwe kuwa kuna mtaalamu wa kuzitumia.
Mgwame ameongeza kuwa hali hiyo inatokana na changamoto waliyokuwa nayo ya kuwa na upungufu wa wataalamu wa kuziendesha mashine hizo hivyo kufanya zoezi kuenda taratibu kushinda ilivyotarajiwa.
Aidha amesema changamoto nyingine iliyojitokeza jana jioni mpaka kupelekea kufungwa kwa vituo hivyo mapema kabla ya wakati ni kukatika kwa umeme na mashine kuishiwa chaji na kuzima hivyo kushindwa kuendelea na zoezi hilo.
Mgwame amesema kuwa licha ya changamoto hizo kujitokeza lakini uandikishwaji huo bado unaendelea vizuri na wananchi wamejitokeza kwa wingi ili kuweza kupata haki yao hiyo ya kujiandikisha.