Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara, John Mnyika
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) leo kimefungua kesi ya kikatiba katika Mahakama ya Afrika Mashariki, wakimshitaki Mwanasheria Mkuu wa serikali nchini Tanzania kwa uvunjaji wa katiba ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuzuia mikutano ya hadhara na ndani ya vyama vya siasa kinyume na mkataba wa uanzishwaji wa Jumuiya hiyo inavyosema.
Aidha mshtakiwa mwingine ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,Balozi Liberat Mfumukeko, ambapo yeye kimsingi kazi yake kusimamia nchi wanachama kuona wanaheshimu mkataba huo.
Akizungumza mara baada ya kufungua kesi hiyo na huku wakisubiri ipangiwe majaji wa kusikiliza kesi hiyo, Mwansheria wa Chadema John Mallya akiwa ameongozana na Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara, John Mnyika, amesema wanaamini mahakama hiyo itatenda haki.
Amesema wamejitahidi kuleta vielelezo vyote vya zuio mbalimbali za polisi zilizofanywa kwa chama hicho Mwanza, Dodoma na hata mahafali ya wanafunzi wa vyuo vikuu ambao ni wanachama wa chama hicho.
Mallya amesema wakati wao wanazuiwa, CCM wanaruhusiwa kufanya shughuli zao za mahafali na mikutano ya hadhara na ndani wakifanya bila zuio la polisi.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, amesema wanaamini uminyaji wa Demokrasia unaofanywa na Rais John Magufuli utapatiwa ufumbuzi, kwani wao kama chama wanaona ni wazi mbinu za kuminya harakati zao za kuingia Ikulu mwaka 2020 na kuihakikishia ushindi CCM mwaka huo.
Amesema Katiba ya nchi hairuhusu kumshitakiwa Rais, lakini ingeruhusu leo angekuwa mshitakiwa wa kwanza, ila kwa niaba yake ndio maana ameshitakiwa Mwanasheria Mkuu wa serikali kwa kuvunja Ibara ya 6 na saba ya mkataba wa uundwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Amesema kesi hiyo ni aibu kwa Rais Magufuli kama Mwenyekiti wa Jumuiya hii kushitakiwa kwa kuvunja katiba ambayo anatakiwa kuwa mstari wa mbele kuisimamia, kwani amekuwa mstari wa mbele kusema haruhusu mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa na amekuwa akirudia rudia.
Amesema Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo anatakiwa kuchunguza ukiukwaji wa mkataba huo na kuhakikisha unaheshimiwa na nchi zote wanachama.
Kuhusu suala la yeye kukaa kimya na watu kuanza kumtafakari tofauti, alisema ni uzushi wa kisiasa na yeye yupo pamoja na chama chake na Ukawa kwa ujumla na anaunga mkono yote wanayokataa kuhusu udikteta wa Bungeni na hata nje ya Bunge na ndio maana ameungana yeye na Mwenyeki wa Chadema Freeman Mbowe kuwa washitakiwa wa kesi hiyo.




