Alhamisi , 11th Mei , 2017

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa pongezi kwa wabunge wake wateule wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kutoka kundi C. Wabunge hao ambao ni Josephine Lemoyan na Pamela Maassay hiyo jana walichaguliwa na Bunge la Tanzania.

Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano cha chama hicho, Tumaini Makene ilieleza kuwa Chama kina imani kubwa kuwa wabunge hao wateule wa EALA watakuwa wawakilishi bora wa nchi yetu kwenye bunge hilo wakizingatia manufaa, maslahi na matakwa ya Watanzania na wananchi wa nchi zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Kupitia uwezo, uzoefu na utayari walionao wa kujifunza na kupokea maarifa mapya, Lemoyan na Maassay watabeba matumaini ya mabadiliko ya Watanzania, ambao wangependa kuona ushirikiano wa EAC unakuwa na nguvu za kiuchumi na kisiasa uliojengwa katika misingi ya kidemokrasia kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi.

“Hivyo, chama kinawaahidi ushirikiano wakati wowote watakapohitaji ili waweze kutimiza wajibu na majukumu hayo kwenye uwakilishi wa EALA na EAC kwa ujumla kwa niaba ya nchi yetu,” - taarifa hiyo iliyotolewa na idara ya habari CHADEMA ilieleza.

Chadema jana imejipatia wawakilishi wanawake wawili katika bunge la Afrika Mashariki ambapo wabunge hao wanakamilisha nafasi tisa zilizokuwa zinahitajika.