Ijumaa , 19th Aug , 2022

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimekemea tabia ya udhalilishaji inayodaiwa kufanywa na baadhi ya watumishi waliopewa dhamana katika halmashauri mbalimbali ikiwemo ya Sikonge mkoani Tabora. 

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho Shaka Hamdu Shaka

Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho Shaka Hamdu Shaka, wilayani Sikonge mkoani Tabora, akiwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM na uhai wa chama mkoani humo na kusema chama hakiungi mkono udhalilishaji wowote na inafuatilia hatua kwa hatua jambo hilo.

"Nataka niseme na hili la udhalilishaji wanawake kingono, nimelikuta Kaliua na lipo Sikonge, lakini hata kwenye maeneo mengine kwa watumishi wa umma, ujumbe umefika, wenye hiyo tabia waache, waache kuwadhalilisha dada zetu, waache kuwadhalilisha mama zetu, waache kuwadhalilisha ndugu zetu wa kike hapa Sikonge, hiyo tabia imeshamiri kwa sababu tu kuna mtu ana dhamana, ana fursa ya kuwasaidia wengine," amesema Shaka.

Aidha Shaka ameongeza kuwa, "Hamuwasaidii mama zetu, hamsaidii dada zetu mpaka muwadhalilishe kingono, chama kinafuatilia kwa karibu sana, hataturahusu udhalilishaji wa aina yoyote kwa wanawake ndani ya nchi hii, wanawake hawa wanauwezo mkubwa sana katika kufungua fursa za maendeleo katika Taifa letu,".