Spika wa Zamani wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Pius Msekwa akiwa na Rais Mstaafu wa awamu ya Pili Hussein Mwinyi.
Akizungumza leo Asubuhi katika kipindi cha East Africa Breakfast, Msekwa amesema kuwa suala hilo lilianza toka mwaka 1995 lakini wanachama walikuwa na mwamko mdogo kujitokeza kuwania nafasi hiyo ila kwa kuwa sasa demokrasia imepanuka ndiyo kumefanya wanachama wengi kujitokea wakati huu.
Mh. Mswekwa amesema baada ya mfumo huo kuanzishwa mwaka 1995 na yeye alikuwa ni mmoja wa watu waliochukua fomu ambapo anasema alifanya hivyo baada ya kushawishiwa na wazee ndani ya chama hicho ili kuleta changamot ya wengine kujitokeza katika Kinyang'anyiro hicho.
Katika hatua nyingine amesema kwa sasa Chama cha Mapinduzi kimepoteza umaarufu wa kisiasa kutokana na wananchi kuonyesha dhidi ya serikali yao kutokana na kashfa mbalimbali kwa baadhi ya viongozi wake ikiwemo ya EPA na Richmond.
Amesema kuwa hali hiyo ya kushuka kwa chama ilijitokeza katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 baada ya mwaka 2005 kushinda kwa asilimia 80 lakini baada ya kashfa hizo ndio chuki kwa wananchi wakaweza kukifanya kushinda kwa asilimia 61.
Kuhusu maamuzi yake aliyoyafanya mwaka 1995 ya kutangaza nia ya kugombea urais wa Tanzania, Msekwa amesema haikuwa matakwa yake, bali alishawishiwa na baadhi ya wazee wa chama atangaze nia ili kuwavutia watu wengine wagombee.
"Wakati ule watu wengi bado walikuwa ni waoga kujitokeza, sasa baada ya muda kupita bila watu kujitokeza, nikafuatwa nikaambiwa mimi spika nitangaze kuwa nagombea, na mimi nikafanya hivyo, lakini ikapita wiki 1, wiki 2 hawajitokezi bado, lakini baadaye wakajitokeza kwa wingi, na hatimaye wakabaki watano, wakabaki watatu na baadaye mmoja na wote walioachwa wakamuunga mkono aliyeteuliwa"