Jumanne , 9th Jun , 2015

Zoezi la uandikishaji katika daftari la kudumu la wapiga kura kwa kutumia mfumo mpya wa BVR mkoani Mwanza, limeanza kwa malalamiko kutokana na baadhi ya vituo kufunguliwa nje ya muda uliowekwa na tume ya taifa ya uchaguzi (NEC).

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Jaji Damian Lubuva

Baadhi ya wananchi wakizungumza na EATV leo katika mtaa wa Nyamazobe kata ya Mkolani wilayani Nyamagana, wamesema wameanza kujipanga vituoni kuanzia saa 10 alfajiri lakini hawakuweza kuandikishwa hadi saa 6:30 mchana.

Mwananchi Godfrey Sibandese amesema zoezi hilo katika mtaa huo limekuwa na athari kwa wananchi kutokana na wengi kuondoka kwenda katika shughuli zao kutokana na kuchelewa kuanza.

Naye Mrisho Mgalula wa mtaa huo, amesema pamoja na kuchelewa kufunguliwa kituo katika mtaa wao, lakini walemavu wajawazito na akinamama wenye watoto hawakupewa kipaumbele cha kuandikishwa mapema.

Mama Halima Maleck amesema msimamizi wa kituo anatakiwa kuzingatia muda wa kufunguliwa kituo, kwani anapochelewa kunasababisha kuwapo na msururu mrefu kutokana na waandikishaji wa daftari hilo kuwa na kasi ndogo.

Mwenyekiti wa mtaa huo, Julias Kihamba, amesema licha ya kituo kuchelewa kufunguliwa, lakini awali kulikuwa na tatizo la mipaka ya mtaa hivyo kuonekana kuchelewesha zoezi hilo.

Msimamizi wa uandikishaji katika kituo hicho, Raphael Anthony, amesema zoezi limechelewa kuanza kutokana na baadhi ya mashine kutokuwa na mitaa hivyo kuathiri kuanza kwa zoezi.

Huko mkoani Shinyanga, mkoa huo unakadiriwa kuandikisha watu 800,000 wote wakiwa na sifa ya kupiga kura katika daftari la kudumu la wapiga kura lililoanza rasmi leo.

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, ally Rufunga, amesema hayo wakati akizindua uandikishaji huo katika kijiji cha Nyandekwa wilayani Kahama, amesema jumla ya vituo 1,000 vimetengwa kwa ajili ya kufanikisha zoezi hilo na kila kituo kimepatiwa vifaa vya kutosha pamoja na elimu kwa waandikishaji.

Amesema wilaya ya Kahama ina vituo 543, halmashauri ya Ushetu vituo 235, Msalala 161 na mji Kahama vituo 157.