Napenda kuwakaribisha kwenye Kikao hiki ambacho nitawaelezea mchakato wa Uandikishaji wa Wananchi wetu katika daftari la kudumu la wapiga kura ambalo tofauti na awamu zilizopita, safari hii uandikishaji utafanyika kwa kutumia teknolojia mpya ya uandikishaji ijulikanayo kama Biometrix Voter Registration (BVR).
2. MAFUNZO
Ndugu Wanahabari,
Mafunzo kwa Watendaji wetu ambao watahusika na zoezi hili tayari yamekwisha fanyika kama ifuatavyo:-
• Mafunzo kwa ajili ya Mratibu wa Mkoa, Maafisa Waandikishaji na Maafisa Waandikishaji wasaidizi ngazi ya jimbo yalifanyika tarehe 27 – 28/04/2015 yakifuatiwa na Mafunzo ya Maafisa waandikishaji ngazi ya Kata yaliyofanyika tarehe 18 – 19/05/2015 kwa Halmashauri zote na mwisho Mafunzo ya BVR Opereta na Waandishi Wasaidizi yaliofanyika tarehe 21 – 22/05/2015.
• Nia kubwa ya Mafunzo haya yalikuwa ni kuwapa uelewa wahusika na hasa namna ya kutumia Teknolojia mpya kwa Mashine zijulikanozo kama BVR Kits lakini vile vile Mfumo mpya utakaotumika.
3. VIFAA
Ndugu Wanahabari,
Katika zoezi hili la uboreshaji wa daftari vifaa mbalimbali vimegawawiwa kwenye Halmashauri zetu na TUME YA UCHAGUZI MKUU. Vifaa hivyo vitagawiwa kwa mujibu wa maelekezo ya Tume kwa kuzingatia idadi ya vituo na idadi ya wapiga kura wanaolengwa kuandikishwa katika maeneo husika. Vifaa hivi vimegawiwa katika hatua mbili. Hatua ya kwanza ni Tume kuvipeleka kwenye Halmashauri na hatua ya pili ni Halmashauri kuvisambaza kwenye Vituo vya kujiandikisha.
Nimeambiwa baada ya zoezi hili kukamilika Afisa Mwandikishaji ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri husika anatakiwa kuvikusanya vifaa vyote na kuvihakiki na kuwasiliana na Tume kwa ajili ya utaratibu wa kuvirudisha Tume. Vifaa hivyo ni:-
1. Fomu: Na1,Na.2 ,Na.3A, Na. 3B, Na.4, Na.5, Na.6, Na.7
2. Bango la Kituo cha kuandikisha wapiga kura
3. Kalamu ya wino mweusi
4. Kadi ya Plastiki (PVC)
5. Begi
6. Boksi
7. Utepe wa gundi
8. Gundi nzito na pini
9. Mfuko mdogo wa plastiki, na
10. Sanduku la vifaa BVR. Vifaa vyote vimeshapelekwa na Halmashauri zote na nimeelezwa wahusika wote wameshapewa maelekezo ya namna ya kutumia vifaa hivyo. Pia kama ilivyosisitizwa vifaa hivi vitunzwe vizuri katika hali ya usafi na usalama. Hatua za Kisheria zitachukuliwa dhidi ya wakaopoteza vifaa hivyo au kuviharibu kwa makusudi.
VITUO VYA KUANDIKISHA
Ndugu Wanahabari
Mkoa wetu una Vituo vya kuandikisha wapiga kura 748 kwa mchanganuo ufuatao:-
• Halmashauri ya Manispaa 218
• Halmashauri ya Wilaya Nkasi 190
• Halmashauri ya Wilaya Kalambo 158, na
• Halmashauri ya Wilaya Sumbawanga 182 , Vituo hivi vimeainishwa na Maafisa waandikishaji na vimesaidia sana hasa kwa TUME kufanya maamuzi mbalimbali kwa kuzingatia vituo hivyo. Kwa utaratibu wa TUME YA UCHAGUZI Vituo vitafunguliwa saa 1.30 asubuhi hadi 12.00 jioni.
6. MAOTEO (PROJECTION) YA WATAKAO JIANDIKISHA
Ndugu Wanahabari,
Maoteo (Projection) ya wanaotegemewa kuandikishwa kwa Mkoa wetu ni kama ifuatavyo:¬-
1. Halmashauri ya Manispaa 107,000
2. Halmashaurii ya Sumbawanga 141,000
3. Halmashauri ya Kalambo 124,000
4. Halmashauri ya Nkasi 152,000
7. SIKU YA KUANZA UANDIKISHAJI
Ndugu Wanahabari,
Kwa mujibu wa ratiba yetu tunategemea kuanza zoezi la kuandikisha wapiga kura kwenye daftari letu la kudumu tarehe 24/05/2015 hadi tarehe 23/06/2015 zoezi hili litakuwa la siku 28. Napenda kuwapa taarifa kuwa vifaa vimeshafika kwenye vituo tayari.
8. SIFA ZA KUANDIKISHWA
Ndugu Wanahabari,
Ili mtu aweze kuandikishwa kuwa mpiga kura anapaswa kuwa na sifa zote zitakazohitajika kwa mujibu wa Sheria. Sheria hizo ni pamoja na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura 343 na Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Sura 292. Kwa mujibu wa Sheria hizo nilizotaja sifa kuu za mpiga kura ni:-
(a) Kuwa raia wa Tanzania, na
(b) Kuwa na umri wa Miaka 18 au zaidi vile vile kwa raia wote watakaokuwa wametimiza umri wa Miaka 18 ifikapo tarehe ya Uchaguzi.
Kwenye kipengele hiki cha sifa mtu anaweza kukosa sifa za kuandikishwa kuwa mpiga kura kwa mujibu wa Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343 Kifungu Na. 11(i) na Sheria ya Serikali za Mitaa Sura 292 Kifungu cha 9 (i) Mtu anakosa sifa za kuandikishwa kwa sababu zifuatazo:-
(i) Ana uraia wa Nchi nyingine
(ii) Amethibitika rasmi kuwa ana ugonjwa wa akili
(iii) Amehukumiwa kifo na Mahakama
(iv) Ametumikia Kifungo zaidi cha Miezi Sita
(v) Amezuiliwa na Sheria kuandikisha kuwa mpiga kura
(vi) Hatakuwa ametimiza umri wa kupiga kura ifikapo tarehe siku ya uchaguzi
9. MAWAKALA WA UBORESHAJI WA DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA NA WATAZAMAJI
Ndugu Wanahabari,
Kwa mujibu wa Kifungu cha 15 (A) (i) cha Sheria ya Uchaguzi Sura 343 na Kifungu cha 17 A (i) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292 vyama vya Siasa vyenye Usajili wa kudumu vinapewa nafasi ya kuteua mtu mmoja kwa wakala wa uboreshaji kwa kila Kituo cha uboreshaji. Kila Chama kitafanya uteuzi wa Wakala husika na kumtaarifu Mwandikishaji kwa maandishi kuhusu uteuzi huo. Mawakala hao watakuwa na wajibu wa kufuatilia zoezi la uboreshaji, kushirikiana na waandishi wasaidizi kutambua wakazi wa eneo hilo na kutoa taarifa juu ya watu wasio kuwa na sifa na kuandika idadi ya watu walioandikishwa na jina la mtu wa Mwisho. Pia Mawakala hawataruhusiwa:-
(a) Kuingilia shughuli za uendeshaji wa zoezi la uboreshaji. Msimamizi wa Kituo ndiye mwenye ya mwisho ya juu ya nani anastahili/ hasitahili kuandikishwa.
(b) Kufanya Kampeni za Kisiasa katika Kituo cha Uandikishaji, na
(c) Kuorodhesha majina ya watu wanao jiandikisha. Natoa wito kwa Mawakala walioteuliwa na Vyama vyao kuzingatia haya vinginevyo atakayekiuka atachukuliwa hatua za Kisheria.
WATAZAMAJI WA ZOEZI LA UBORESHAJI
Ndugu Wanahabari,
Kutakuwepo na watazamaji wa Ndani na Kimataifa wanaoruhusiwa kutazama mchakato wa uboreshaji utakaofanyika katika vituo mbalimbali. Watzamaji kabla ya kutembelea Vituo mbalimbali vya uandikishaji ni lazima wapewe idhini na Tume ya Uchaguzi. Mpaka sasa Mkoa wa Rukwa umepokea watazamaji wa ndani watatu (3) na wanazo barua za Tume ambazo wameziwasilisha kwa Maafisa waandikishaji.
WITO WANGU
Ndugu Wanahabari,
Na Maafisa wa Tume, napenda kuchukua fursa hii kuwaomba
Kwanza, Wananchi kuwa watulivu wakati wote wa zoezi
Pili, kuwatakia watendaji wote wa Tume kuzingatia Miongozo waliopewa
Tatu, kuvitaka vyama vyote vya siasa kufuata utaratibu uliwasilishwa na Tume kwenye zoezi hili na kuwa kamwe zoezi hili lisitumike kupotosha watu. Watu waachiwe wajiandikishe kwa HIARI na UTASHI unaozingatia Sheria ya nilizotaja hapo juu.
Nne, Changamoto yoyote itakayojitokeza iripotiwe mapema kwa Maafisa waandikishaji na Mratibu wa Mkoa ili iweze kuripotiwa kwenye TUME ili ipatiwe ufumbuzi.
Tano, Vyama vihamasishe watu kwa kuzingatia Sheria zilizowekwa na TUME na Serikali kwa ujumla.
Mwisho,
Nichukue fursa hii kuwatakia wananchi ushiriki unaozingatia Sheria na unaoendelea kudumisha mshikamano, umoja na Amani tuliyo nayo.
IMETOLEWA LEO TAREHE 23/05/2015 NA:
Eng. Stella M. Manyanya
Mkuu wa Mkoa
RUKWA