Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli muda mfupi baada ya kuapishwa kwake hii leo, tayari ameanza kazi, ambapo kazi ya kwanza aliyoanza nayo ni uteuzi wa mwanasheria mkuu wa serikali.
Kwa mujibu wa katibu mkuu Kiongozi, balozi Ombeni Sefue, Rais Magufuli amemteua bwana George Mcheche Masaju kuwa mwanasheria mkuu wa serikali, na ataapishwa kesho katika viwanja vya ikulu.
George Masaju ndiye aliyekuwa Mwanasheria mkuu wa serikali ya awamu ya nne ambapo Balozi Sefue amesema kuwa kwa mujibu wa katiba, Rais wa awamu ya tano anayo mamlaka ya kufanya uteuzi huo.
Katika hatua nyingine Rais Magufuli ametangaza kuitisha bunge la 11, Novemba 17 mwaka huu.
Balozi Sefue amesema kuwa Bunge hilo litaanza kikao chake cha kwanza katika tarehe hiyo kwa zoezi la kuapishwa wabunge, na siku mbili baadaye yaani tarehe 19 Novemba jina la waziri mkuu litapelekwa bungeni kwa ajili ya kupitishwa na bunge.