Jumanne , 5th Aug , 2014

Bunge Maalum la Katiba nchini Tanzania limeanza leo vikao vyake vya kupitia na kujadili pamoja na kuboresha rasimu ya pili ya katiba katika mchakato wa kuandika Katiba mpya.

Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba nchini Tanzania, Mh. Samuel Sitta.

Vikao vya leo vimeendelea bila kuwepo kwa wajumbe wa kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ambao wamesusia rasmi vikao vya bunge hilo.

Akifungua bunge hilo hii leo mjini Dodoma Mwenyekiti wa Bunge hilo Mhe. Samwel Sitta amesema kwa mujibu wa sheria ya kikao hicho kuhudhuriwa na zaidi ya robo tatu ya wajumbe inaruhusu kuweza kuendelea na mchakato wa kujadili rasimu hiyo.

Aidha katika hotuba yake ya ufunguzi Mhe. Samwel Sitta amesema wataanza kwa kubadilisha kanuni ili ziweze kusimamia nidhamu na pia kumaliza mchakato huo kwa wakati, kwa kuwa sasa hayuko tayari kumuomba tena Rais aongeze muda baada ya kufanya hivyo katika awamu ya kwanza.

Akichangia katika mabadiliko hayo ya kanuni mjumbe wa bunge hilo Hamad Rashid kutoka Chama cha Wananchi (CUF) amesema rasimu ya Katiba ni mali ya Bunge kwa hiyo lina mamlaka ya kubalisha chochote kwa kupiga kura, na hivyo kuwataka ambao hawajarejea bungeni waache kuupotosha umma.