Jumamosi , 28th Jun , 2014

Kamati ya bunge ya Bajeti imekataa kubariki Muswada wa Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani VAT na Muswada wa Sheria ya utawala wa kodi ambao ulikuwa uwasilishwe bungeni jumatatu ijayo na kujadiliwa ili misamaha ya kodi isiyo na tija ifutwe.

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Spika wa Bunge Anna Makinda alitangaza hatua hiyo jana na kusema kuwa Kamati imeona miswada hiyo isiwasilishwe bungeni kwa kuwa inagusa sekta nyingine ambazo wadau wake hawajashirikishwa.

Baada ya kauli hiyo ya Spika Makinda, Naibu waziri wa fedha Mwigulu Nchemba alisema hata baada ya muda huo kusogezwa mbele hakuna jambo jipya litakalofanyika kwa kuwa miswada hiyo ilipita katika ngazi ya makatibu wakuu wa serikali ambao walishirikisha wataalamu na wadau wa sekta husika na baada ya hapo makatibu hao na wataalamu wakashiriki wakati Miswada hiyo ilipopitishwa na Baraza la Mawaziri.

Naibu Waziri aliongeza kusema kwamba anachokiona ni kucheleweshwa kwa mambo ambayo yalitakiwa kufanyika ili kuharakisha kuleta maendeleo na kutoa mfano wa Ramani ya Mji wa Dodoma ambayo Nigeria waliichukua na kuitumia kujenga mji mkuu wa nchi hiyo Abuja, huku Tanzania ikibakia na ramani bila mji.

Aliwakumbusha wabunge kuwa mara kwa mara wamekuwa wakiitaka Serikali ilete Muswada wa Sheria utakaofuta misamaha ya kodi ambayo imekuwa ikiikosesha Serikali fedha za maendeleo na sasa umeletwa bungeni na unapigwa kalenda.