Jumatano , 27th Aug , 2014

Ofisi ya Bunge Maalum la Katiba mjini Dodoma, imetoa ufafanuzi juu ya taarifa zilizotolewa kwenye vyombo vya habari kuhusu kuchelewa kwa malipo ya posho za Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba na kusema taarifa hizo za upotoshaji.

Spika wa Bunge Maalumu la Katiba Samuel Sitta.

Mkurugenzi wa Habari na Itifaki Bw. Jossey Mwakasyuka ameeleza hayo jana wakati alipokutana na waandishi wa habari na kusema kuwa Wajumbe wote wa Bunge Maalum ambao wanahudhuria vikao vinavyoendelea wameshalipwa posho zao zote kama wanavyostahili.

Mwakasyuka ameongeza kuwa,ofisi ya Bunge Maalum imekerwa na kuchapishwa kwa taarifa hizo na baadhi ya vyombo vya habari kwani taarifa hizo ni za upotoshaji na zina lengo la kuwadhalilisha wajumbe na kuwafanya waonekane wenye kuishi na kufanya kazi kwa kutegemea posho.

Mwakasyuka ameongeza kuwa, si vema kwa vyombo vya habari kuwadhalilisha wajumbe hao kwa njia yoyote ile kwani kwa kufanya hivyo kunawavunja moyo na kuwafanya washindwe kuifanya kazi ya Bunge Maalum vizuri kama ilivyotarajiwa na wananchi.