Alhamisi , 21st Jan , 2016

Mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi ya CCM Abdallah Bulembo amewaambia walimu wakuu wa shule za sekondari zinazomilikiwa na jumuiya hiyo kama hawawezi kazi waache kazi kuliko kuingiza siasa kwenye ukusanyaji wa mapato ya jumuiya hiyo.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa Abdullah Bulembo

Aidha alisema kuwa endapo kuna shule yoyote inayomilikiwa na jumuiya hiyo itakaguliwa na kuonekana kuna ubadhirifu atahakikisha kuwa mkuu wa shukle husika anafikishwa mahakamani.

Bulembo ametoa kauli hiyo leo wakati akifungua kikao cha kazi cha kamati ya utekelezaji na baraza kuu la wazazi la jumuiya hiyo kilichokuwa na lengo la kuweka mikakati, maazimio na maamuzi kuhusiana na jumuiya hiyo.

Amesema kuna baadhi ya walimu wakuu ambao wamekuwa hawapeleki michango inayokusanywa bila ya kuwa na sababu zozote za msingi na kwamba kama kuna mwalimu hawezi kukusanya michango ni bora aache kazi.

Kikao hicho ambacho pia kimewahusisha makatibu wa mikoa wa jumuiya ya wazazi kimelenga kuhakikisha kuwa fedha zote zinazotozwa kwenye shule za jumuiya hiyo kwa ajili ya kupelekwa makao makuu yajumuiya hiyo zinapelekwa kwa wakati.