Jumanne , 8th Dec , 2015

Mbunge wa jimbo la Bunda mjini mkoani Mara, Esther Bulaya, anatarajiwa kutinga mahakama kuu kanda ya Mwanza leo jumanne baada ya kufunguliwa kesi ya madai ya kupinga matokeo yaliyompa ushindi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.

Mbunge wa jimbo la Bunda mjini mkoani Mara, Esther Bulaya

Kesi hiyo ya madai imefunguliwa Novemba 19, mwaka huu na Magambo Masato na wenzake 30, ikipinga matokeo yaliyompa ushindi bulaya pamoja na wenzake 20 akiwamo mkurugenzi wa wilaya ya Bunda ambaye alikuwa msimamizi wa uchaguzi na mwanasheria mkuu.

Katika matangazo yaliyowekwa katika ubao wa matangazo ya mahakama kuu kanda ya Mwanza, waomba maombi wanadai upatikanaji wa ubunge wa Bulaya haukuwa halali kutokana na kukiukwa kwa baadhi ya mambo.

Taarifa hiyo imedai msimamizi wa uchaguzi hakutakiwa kumtangaza bulaya kuwa mbunge halali wa jimbo hilo kutokana na kwenda kinyume na sheria pamoja na kanuni za uchaguzi huo.

Kesi hiyo ni moja ya kesi zilizofunguliwa kupinga matokeo ya ushindi wa baadhi ya wabunge katika majimbo mbalimbali nchini tangu uchaguzi mkuu ufanyike oktoba 25, mwaka huu.