Ijumaa , 10th Jul , 2015

Hospital ya rufaa ya mkoa wa Tanga Bombo kwa kushirikiana na shirika la Interplast la Ujerumani wamewataka wanachi wa jiji la Tanga wenye matatizo ya maumbile kujitokeza katika zoezi la huduma ya upasuaji wa kurekebisha maumbile.

Hospital ya rufaa ya mkoa wa Tanga Bombo.

Akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya mganga mkuu daktari Wallece Karata amesema jopo la wataalam saba wakiungana na timu ya hospital ya bombo wamejiandaa kutoa huduma hiyo kwa muda wa siku 12 ili kurekebisha maumbile yaliyokuwa tofauti katika miili ya binadam.

Daktari huyo amesema watu wote watakaojitokeza watapatiwa matibabu kutegemea na matatizo yao ambapo amesema kuwa zoezi hili ni mara ya nne kufanyika mkoani hapa.

Aidha amesema huduma ya upasuaji wa kurekebisha maumbile watakayoifanya ni pamoja na upasuaji wa uvimbe, Midomo Sungura kupasuka, kaakaa la kinywa, maziwa makubwa kwa wanaume, vidole pacha, uvimbe wa kujaa damu ndani pamoja na vipele sugu vya tangu kuzaliwa.

Huduma ya upasuaji wa kurekebisha maumbile inatarajiwa kuanza Agost 3 Mwaka huu hadi Agosti 14 mwaka huu katika hospital ya Bombo kwa gharama za shilingi elfu tano na matibabu yatakuwa ni bure ikiwa zoezi la kujiandikisha kwa ajili ya kupata huduma hiyo linaendelea hadi Julai 31.