Jumatatu , 11th Jul , 2022

Bodi ya Maji ya bonde la Wami Ruvu wametoa msaada wa mifuko ya saruji 50 kwa shule ya msingi Kidunda iliyopo Kata ya Mkulazi, Halmashauri ya wilaya ya Morogoro. Msaada wa mifuko hiyo ni kutelekeleza agizo la Waziri wa Maji Jumaa Aweso, alilotoa alipofika katika Kijiji hicho.

Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki Hamis Taletale, akipokea mifuko ya saruji iliyotolewa na Bodi ya Maji ya bonde la Wami Ruvu

Mhandisi Mmasy amesema Bodi hiyo ilipewa maagizo ya kutoa mifuko ya saruji 50 na DAWASA mifuko 50 ili kuunga mkono juhudi za wananchi wa eneo hilo na kuendelea kulinda vyanzo vya maji ambavyo vimekua tegemezi kwa wakazi wa mikoa ya Morogoro, Pwani na Dar es Salam

"Mheshimiwa Waziri wa Maji Jumaa Aweso, aliona kuna umuhimu wa sisi kusaidia shule hii mifuko hii 50 ya saruji hivyo naamini itasaidi katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya shule hii na kupunguza adha wanazopata wanafunzi,"amesema Mmasy

Akipokea mifuko hiyo Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki Hamis Taletale, maarufu kama Babu Tale amemshukuru Waziri wa Maji Jumaa Aweso kwa kutimiza ahadi yake kupitia Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu

Babu Tale amesema  kupatikana kwa mifuko hiyo imeleta chachu kwa wananchi kuendelea kuiamini serikali ya awamu ya sita huku akimpongeza Rais Samia, kwa kuendelea kuwaletea maendeleo wananchi wa jimbo hilo ikiwemo kupatikana kwa kituo cha afya Mkulazi .