Wizara ya Nishati na Madini nchini Tanzania imetumia zaidi ya shilingi bilioni saba kwa ajili ya ruzuku kwa wachimbaji wadogo wa madini nchini, lengo likiwa ni kuwajengea uwezo ili wafanye shughuli za uchimbaji kitaalamu zaidi.
Msemaji wa wizara hiyo Bi. Badra Masoud ameiambia Hotmix kuwa fedha hizo zimetolewa chini ya mradi unaosimamiwa kwa pamoja na Benki ya Dunia na kwamba fedha zaidi zimepangwa kutolewa katika awamu nyingine inayoanza mwaka huu.
Ukiachilia mbali wachimbaji wadogo, Bi. Badra amesema ruzuku hiyo imehusisha pia watoa huduma katika migodi inayomilikiwa na wachimbaji hao, wakiwemo akina mama lishe pamoja na watu wote wanaouza vitu na kutoa huduma katika maeneo ya wachimbaji wadogo wadogo.