Akizungumza wakati wa kuhitimisha ziara yake ya siku 4 mkoani humo Makamu wa Rais Dkt. Mpango amesema, ameshtushwa na taarifa iliyotolewa na Waziri Bashe na anaagiza hatua za uchunguzi kufanyika na vyombo vya dola viwasake waliohusika.
Amesema fedha hizo zilizopigwa ni mikopo ya wakulima wa Kisanga Amcos Sikonge mkoani Tabora.
"Asante Waziri Bashe kwa kulipua hili na hongera kwa kuchukua hatua kwako kwa kuwasimamisha kazi maafisa kilimo na ushirika, namuagiza Mtenda Mkuu wa NMB huyu Afisa Mikopo Tabora aliyekula njama za wizi huu asimamishwe kazi mara moja na watumishi wa umma wote waliopiga fedha hizo na wengine kuhamishwa wasakwe na kushikiliwa kwa uchunguzi," Ameagiza Makamu wa Rais
Dkt.Mpango amesema ni jambo la aibu na ukosefu wa maadili kuona walioshiriki wizi huo ni watumishi wa umma tena wanawaibia wanyonge ambao ni wakulima.
Hatua hiyo, imefikiwa baada ya Waziri wa Kilimo Hussein Bashe, kuwalipua waliohusika katika ubadhilifu wa fedha za tumbaku sh. Bilioni 1.2 na kusisitiza kuwa wizi huo umefanywa bila woga na watumishi walioshiriki wapo kazini.
Waziri Bashe amesema watuhumiwa hao walikuwa wajanja, kwani hakuna uingizaji wa fedha wa moja kwa moja uliofanywa unaoweza kuonekana kutoka kwenye akaunti ya chama kwenda kwenye akaunt zao, lakini akaunti zao zilikutwa na fedha nyingi na miamala ilibainika kuingia kama cash bila chanzo kujulikana.
"Baada ya vyombo vya usalama na TAKUKURU kuwabana viongozi wa chama walikiri kuwa walikuwa wanashiriki biashara hiyo na watumishi wetu kwa usaidizi wa Afisa Mikopo wa NMB," amesema Waziri Bashe