Jumatano , 14th Jan , 2015

Kamati ya bunge ya hesabu za serikali za mitaa (LAAC) imebaini ufisadi wa zaidi ya shilingi Bilioni 1.7 katika jiji la Dar es Salaam na kuiagiza TAMISEMI kufuatilia kashfa hiyo.

Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya bunge ya hesabu za serikali Mh Rajab Mbarouk Mohamed

LAAC imebaini ufisadi wa zaidi ya shilingi bilioni moja nukta saba katika jiji la Dar es Salaam na kuiagiza wizara ya tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) kufuatilia kashfa hiyo na kuwachukulia hatua za kinidhamu watendaji wote waliohusika katika upotevu wa fedha hizo.

Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya bunge ya hesabu za serikali Mh Rajab Mbarouk Mohamed amemtaka waziri mwenye dhamana na wizara hiyo Mh Hawa Ghasia kuwachukulia hatua wote waliohusika katika kutoweka kwa fedha hizo.

Pia ameongeza kuwa kukosekana kwa utashi wa kuchukua tahadhari katika mikataba inayoingiwa na wabia sambamba na kile alichokiita kubinafsisha manispaa kwa watendaji kunasababisha kutoa mwanya wa kufanyika kwa ubadhirifu.

Aidha suala la baadhi ya watendaji wa manispaa kukaimishwa ofisi kwa muda mrefu nalo limeibuliwa na kamati hiyo jambo linalodaiwa kutoa mwanya wa baadhi ya watendaji wasio waaminifu kuutumia mwanya huo kuchota fedha za miradi mbalimbali ambapo waziri wa TAMISEMI Mh Hawa Ghasia amezitupia lawama hizo kwa watendaji wakuu wa manispaa kwa kutotekeleza ipasavyo wajibu wao.

Kuhusu suala la uchafu katika jiji la Dar es Salaam mkurugenzi mtendaji wa jiji la Dar es Salaam Bw Wislon Kabwe amesema linakwama kutekelezeka kwa kiwango cha juu kutokana na manispaa za jiji la Dar es Salaam kugoma kutoa ushuru utakaowezesha kuondolewa kwa ufanisi taka hizo kwa muda wa miaka mitatu hadi minne mpaka sasa jambo linalokwamisha uzoaji wa taka kwa wakati katika jiji hilo.