Jumanne , 4th Oct , 2022

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga amesema atahakikisha fedha zote zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mapya 191 kwenye shule za sekondari mkoani humo zinatumika kama ilivyokusudiwa ili wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2023 waweze kuanza masomo yao kwa wakati.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga

Serikali ya Awamu ya Sita imeupatia mkoa wa Rukwa shilingi Bilioni Tatu na Milioni Mia Nane na Elfu Ishirini (3,820,000,000/-) kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vipya vya madarasa katika halmashauri nne za mkoa wa Rukwa ambapo kila darasa litajengwa kwa shilingi Milioni Ishirini kupitia mfumo wa “Force Account”.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Sumbawanga Mhe. Sendiga amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha wanafunzi wote wanapata mahala bora na salama kusomea.

“Natoa wito kwa Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi kufuatilia kwa ukaribu ujenzi wa madarasa hayo ili yaweze kukamilika kwa muda yaani ndani ya siku Sabini na Tano (75) kama alivyoelekeza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI na kwa ubora ulioelekezwa pamoja na kukamilisha utengenezaji wa madawati yake” alisisitiza Sendiga.